Articles
Harambee uchangiaji mradi wa simbo za posta na anuani za makazi
Ndugu Waandishi wa Habari,
Utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi na simbo za posta ulianza kwa majaribio katika Manispaa ya Arusha mwaka 2009 ambapo eneo kubwa ndani ya Kata 8 zimewekwa majina ya mitaa na namba za nyumba. Kata hizo ni Sekei, Kati, Levolosi, Kaloleni, Themi, Unga Limited na Olorieni, na tayari nyumba zipatazo 5,000 zimeshawekewa namba.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kufuatia mafanikio ya utekelezaji wa mfumo huu kwa majaribio katika Manispaa ya Arusha, utekelezaji wa awamu ya kwanza umeanza mwaka 2011 katika Manispaa ya Dodoma ambapo eneo kubwa katika Kata 8 pia zimewekwa majina ya mitaa na tayari nyumba zipatazo 7,500 tayari zimeshawekewa namba. Kata zilizohusika katika utekelezaji wa mfumo huu katika Manispaa ya Dodoma ni Kilimani, Tambukareli, Madukani, Uhuru, Viwandani, Majengo, Kiwanja cha Ndege na Makole.
Utekelezaji wa awamu ya kwanza unaendelea kwa Manispaa na Halmashauri zingine hapa nchini, ambapo kwa mwaka huu wa fedha utekelezaji unatarajiwa kufanyika katika Manispaa zote za Mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar. Utekelezaji katika Manispaa/Halmashauri nyingine utafuata. Ndugu Waandishi wa Habari, Mfumo wa anuani za makazi na simbo za posta ni mtambuka. Hivyo, utekelezaji wake unahitaji ushirikiano mkubwa na wa karibu kutoka kwa wadau mbalimbali.
Kwa mfano, Sera ya Taifa ya Posta inaelekeza uanzishwaji wa anuani za makazi na postikodi, wakati huo huo mamlaka na madaraka ya uwekaji wa majina ya mitaa na namba za nyumba, kisheria liko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) ambapo utekelezaji wake unafanyika katika ngazi za Halmashauri. Hivyo, ni dhahiri kuwa kunahitajika ushirikiano mkubwa na wa karibu wa wadau mbalimbali katika kutekeleza mfumo wa anuani za makazi na postikodi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Anuani za makazi ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi yetu, kiuchumi, kibiashara, kisiasa, na utoaji wa huduma mbalimbali za jamii. Faida za kuwa na anuani hizi zinamgusa kila mmoja wetu, kuanzia Serikali na taasisi zake, kampuni kubwa na ndogo, wafanya biashara, watoa huduma mbalimbali za jamii (umeme, maji, gesi, huduma za kifedha kama mabenki, wasambazaji wa barua na vifurushi), ulinzi na usalama wa raia watoa huduma za dharura kama vile zimamoto na magari ya wagonjwa, na wananchi wenyewe kwa ujumla.
Faida za kuwa na anuani za makazi na simbo za posta kwa Serikali ni msingi wa kutoa vitambulisho vya kitaifa kwa watanzania; unaongeza ufanisi katika usimamizi ya makazi ya watu; unawezesha kutambua mali na kaya katika eneo husika; utaongeza tija katika huduma za uokoaji na maafa; unawezesha ukusanyaji wa kodi mbalimbali kwa urahisi na kwa wakati; unajenga umoja, mshikamano na utaifa katika nchi; unaongeza kasi ya kupambana na uhalifu, kuimarisha shughuli za uhamiaji na kuongeza utalii.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa upande wa huduma za posta, utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi na simbo za posta, utarahisisha uchambuaji wa barua kuwa wa haraka na ufanisi zaidi; utawezesha utambuaji wa anuani kwa urahisi zaidi; utaongeza ufanisi katika usafirishaji na usambazaji wa barua na pia vifurushi; utaongeza ufanisi katika kushughulikia malalamiko ya wateja; utapunguza uwezekano wa barua kupotea. Pia una manufaa kwa jamii kama vile; kutoa anuani ya uhakika kwa kila mwananchi au mkazi; itarahisisha utoaji wa utambulisho sahihi; unarahisisha kupata huduma za jamii kama vile za afya, usalama, maji; kuwezesha matumizi ya vifaa vya kisasa (kwa mfano vifaa vya kuongoza magari kwa kutumia mfumo wa GPS) katika miji yetu; unarahisisha biashara kwani inawezekana kununua bidhaa ukiwa nyumbani kwa kutumia teknolojia za kisasa kama biashara mtandao; Kutambua mazingira yetu kirahisi na kufahamu mahali ulipo.
Kwa upande wa wenzetu wafanyabiashara, anuani za makazi na simbo za posta zitaboresha maendeleo ya biashara; kupata anuani za kuaminika za wateja; kuwezesha kutoa mikopo na kukusanya madeni kirahisi hasa kwa mabenki; utawezesha uendeshaji biashara kwa njia ya mtandao; Itawezesha upangaji wa mauzo, na utoaji wa matangazo na uhamasishaji katika maeneo ya biashara kwa kuwafikia kirahisi walengwa; kufanikisha kazi za tafiti za biashara, kwa mfano, kuwajua wateja wa tabaka fulani na kuwahudumia ipasavyo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika kutekeleza mfumo wa anuani za makazi na postikodi, ziko pia changamoto. Baadhi ya changamoto hizo ni kuwa na maeneo ambayo hayajapangwa vyema katika miji yetu, usimamizi wa miundombinu ya anuani za makazi na pia uhaba wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mfumo huu kwa haraka ili uweze kuleta maendeleo haraka zaidi. Kwa kutambua umuhimu wa anuani za makazi lakini pia changamoto ya uhaba wa fedha za kutekeleza mfumo huu katika Mkoa wa Dar es Salaam, Viongozi wa Mkoa wa Dar es salaam walikubaliana kwa pamoja kuwa kiandaliwe chakula cha hisani cha kuweza kuchangisha na kupata fedha za kusaidia utekelezaji wa mfumo huu kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa katika Mkoa wa Dar es Salaam. Hivyo, Inatarajiwa kuwa shughuli za uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mfumo utafanyika hivi karibuni katika Viwanja vya Karimjee baada ya maandalizi muhimu kukamilika.
Ndugu Waandishi wa Habari, Serikali, kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, imefungua akaunti maalum ya benki kwa ajili ya uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mfumo wa anuani za makazi katika Mkoa wa Dar es Salaam. Akaunti hiyo inaitwa TCRA – POSTCODE PROJECT yenye namba 0150315694502 iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City.
Ninatoa wito kwa wadau wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuchangia kupitia akaunti hii ili tuweze kutekeleza mfumo wa anuani za makazi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa taarifa zaidi wasiliana na Ofisi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia; Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Ofisi ya Postamasta Mkuu, Shirika la Posta Tanzania na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Asanteni sana kwa kunisikiliza


